Kocha mkuu wa timu ya taifa ya Misri Hector Cuper, amethibitishiwa na uongozi wa chama cha soka nchini humo EFA, bado ana nafasi ya kuendelea kufanya kazi zake kwa uhuru, licha ya kushindwa kutwaa ubingwa wa Afrika siku ya jumapili.
Rais wa chama cha soka nchini Misri (EFA), Hany Abo Rida amezungumza na waandishi wa habari na kueleza kuwa, bado wana matumaini makubwa na kocha huyo kutoka nchini Argentina.
Hany amesema bado wana nafasi nzuri ya kufuzu fainali za kombe la dunia za mwaka 2018 zitakazofanyika nchini Urusi, hivyo wanaona kuna umuhimu wa kuendelea kufanya kazi na Cuper.
Katika harakati za kuwania kufuzu fainali za kombe la dunia za mwaka 2018, Misri wamepangwa katika kundi J sambamba na Niger, Tunisia na Swaziland.
Kocha Hector Cuper amekua hana bahati ya kushinda michezo ya hatua ya fainali, na mchezo wa juzi dhidi ya Cameroon ulikua watano kwake kushindwa kufikia malengo.
Alipokua meneja wa klabu ya Valencia ya nchini Hispania Hector Cuper aliwahi kupoteza michezo miwili ya fainali ya ligi ya mabingwa barani Ulaya, kisha alipoteza mchezo wa fainali ya kombe la Mfalme dhidi ya FC Barcelona alipokua mkuu wa benchi la ufundi la Real Mallorca na baadae lifungwa mchezo wa kombe la washindi dhidi ya SS Lazio.