Kocha wa Mabingwa watetezi wa Kombe la Ligi Kuu Uingereza, Leicester City, Claudio Ranieri ameonesha kuchoshwa na uvumilivu alioutunza kwa muda mrefu kutokana na vipigo mfululizo anavyopokea.

Ranieri ambaye amekuwa akiwalinda kwa heshima kubwa wachezaji wake waliompa ubingwa msimu uliopita, ametishia kufanya mabadiliko baada ya kichapo cha 2-0 dhidi ya Swansea, Jumapili iliyopita.

Kocha huyo ambaye bodi ya Leister ilimpa kura ya kuwa na imani naye licha ya timu hiyo kuendelea kuporomoka kutoka ubingwa hadi nafasi ya 17 ikiwa na pointi 24, amesema kuwa uvumilivu umemshinda na sasa anadhani ni muda wa kufanya mabadiliko.

“Ni ngumu pale unapokuwa umefanikisha kitu fulani kizuri sana na unataka kuwapa tena, nafasi mbili, nafasi tatu. Labda sasa, imezidi,” alisema Renieri.

“Ni kitu ninachoweza kukibadili kwasababu kwa namna hii haitawezekana kuendelea. Huwa ninajiuliza… lakini wakati wote nasema, ‘tunaweza kufanya kitu fulani kizuri,” aliongeza.

Ni kama Leicester ilikumbwa na bahati nzuri nzito mwaka jana lakini ikaitua na kubeba gunia la mkosi wa kuandamwa na vipigo visivyoisha. Huenda kila anayekutana na timu hiyo hukamia kwani anajua anakutana na mabingwa watetezi hali inayoigharimu klabu hiyo.

Timu hiyo ya ‘Mbweha wa King Power’ imeingia kwenye rekodi mbaya ya kuwa mabingwa watetezi waliopoteza michezo mitano mfululizo, tangu majanga kama hayo yalipoikuta Chelsea mwaka 1956.

Picha: Yanayojiri awamu ya tatu majina ya watuhumiwa madawa ya kulevya
Dr Phillip Chiyangwa: Tuna Imani Na Ahmad Ahmad