Shirikisho la soka barani Afrika CAF, limelionya baraza la vyama vya soka kusini mwa Afrika COSAFA, kufuta mipango yake ya kufanya vikao na mabaraza mengine ya soka barani humo.
COSAFA wameonyesha kuwa mstari wa mbele kuhakikisha rais wa sasa wa CAF Issa Hayatou hashindi katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu, ambao umepangwa kufanyika mwezi ujao mjini Adis Ababa nchini Ethiopia.
Mwenyekiti wa COSAFA Phillip Chiyangwa, anatajwa kuwa kiongozi wa mapambano hayo na tayari imebainika amepanga kukutana na viongozi wa mabaraza mengine ya soka ya Afrika Februari 24 mjini Harare nchini Zimbabwe.
Tayari COSAFA imeshamteua mwenyekiti wa chama cha soka nchini Madagascar Ahmad Ahmad, kuwa mgombea pekee wa nafasi ya urais wa CAF kutoka ukanda wa kusini mwa Afrika.
CAF wametoa onyo kwa COSAFA kwa kuwaeleza kuwa, ni lazima waufahamishe uongozi wa juu wa shirikisho hilo kuhusu vikao vitakavyoendeshwa, na wamesisitiza ni lazima utaratibu ufuatwe.