Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Ilala Charles Kuyeko amehaidi kufanya kikao maalum kwaajili ya kuzungumzia miradi ya Halmashauri hiyo ili waweze kukusanya mapato yenye tija kwa Halmashauri hiyo.
Meya amesema hayo katika kikao cha baraza la Madiwani katika Halmashauri hiyo kilicho fanyika leo Februari 15, 2017, ambapo hatua hiyo ni kufuatia mchango wa mbunge wa jimbo la Segerea, Bonnah Kaluwa kuitaka Halmashauri kuweka utaratibu utakao walinda bodaboda licha ya kuwafanya wao ndiyo chanzo cha mapato, ukizingatia Serikali imesitisha ajira kwa sasa.
Aidha, baraza hilo limezungumzia matokeo mabovu ya kidato cha nne kwa shule za Mbondole, Kitonga na Nyeburu ambapo Mbunge wa jimbo la Ukonga Mwita Waitara amezitaja sababu za miundombinu ndiyo iliyopelekea wanafunzi wa shule hizo kufeli kwani zipo mbali na wanafunzi wengi wanao soma hapo, sababu inayopelekea wengi kutokwenda shule kwa kukosa nauli, kwakuwa usafiri mkubwa unatumika ni bodaboda kutokana na miundombinu isiyo rafiki.
Pia Mbunge huyo amewataka wazazi kutoichukulia vibaya dhana ya elimu bure kwa kuitupia mzigo Serikali kwani nao wanapaswa kushiriki kwenye shughuli za maendeleo ya elimu ikiwemo kuchangia ujenzi wa uzio na mambo yenye tija kama hayo.