Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Simon Sirro amesema kuwa vipimo vya Mkemia Mkuu wa Serikali vimebaini mfanyabiashara mkubwa ambaye pia ni mwenyekiti wa klabu ya Yanga, Yusuf Manji hutumia dawa za kulevya.

Akizungumza leo na E-FM, Kamanda Sirro amesema kuwa hali ya Manji ambaye alilazwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kitengo cha moyo, muda mfupi baada ya kuhojiwa na jeshi hilo inaendelea vizuri na kwamba kesho atafikishwa mahakamani akikabiliwa na kesi ya matumizi ya dawa za kulevya.

Kamanda Sirro ameeleza kuwa Manji ameruhusiwa kutoka hospitalini na kwamba amerudishwa katika selo za polisi akisubiri kufikishwa mahakamani.

“[Manji] yuko vizuri na kesho atapandishwa mahakamani kwa kosa la matumizi ya dawa za kulevya,” kamanda Sirro ameiambia E-FM.

“Nitawambia vizuri kesho kwa kuwa kesho ndio nakutana na waandishi wa habari. Kwahiyo wanivumilie, kesho nitawaambia hali halisi ilivyo na wajue mwenyekiti wao ni nani na ni mtu wa namna gani,” ameongeza.

Kamanda Sirro amefafanua kuwa ingawa mfanyabiashara huyo atapandishwa mahakamani kesho, haitamzuia yeye kutolea ufafanuzi tuhuma zinazomkabili.

Aidha, ameeleza kuwa mbali na Manji, Jeshi hilo linawashikilia wasanii kadhaa na watu wengine ambao watafikishwa kesho mahakamani wakikabiliwa na kesi ya matumizi ya dawa za kulevya.

Manji alifika katika kituo cha polisi Alhamisi iliyopita akiitikia wito wa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda aliyemtaja kati ya watu kadhaa wanaotuhumiwa kujihusisha na dawa za kulevya.

Mwenyekiti huyo wa Yanga ambaye awali alikanusha vikali tuhuma dhidi yake, aliwasili katika kituo polisi cha kati jijini Dar es Salaam akisindikizwa na mashabiki wa timu hiyo. Alihojiwa na kufanyiwa vipimo kabla hali yake haijabadilika na kulazwa katika hospitali ya Muhimbili.

 

Wabunge Zanzibar wacharuka, watunga sheria kumdhibiti Maalim Seif
Video: Mpina atoa siku thelathini kwa Kampuni ya Red Sea kubomoa ukuta wake