Kampuni ijulikanayo kwa jina moja la Red Sea iliyopo Keko Gerezaji Jijini Dar Es Salaam, Imepewa mwezi mmoja wa kubomoa ukuta uliojengwa juu ya Mtaro wa maji machafu ambao pia ni eneo chepechepe, ambao unasababisha usumbufu kwa wakazi wa maeneo hayo na kuhatarisha hali ya kiafya wakati wa mvua

Agizo hilo limetolewa na Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, Luhaga Mpina alipokuwa akifanya ziara ya utekelezaji wa maagizo yake ya ziara aliyoifanya mwaka jana.

Kampuni hiyo imepewa  muda huo wa kubomoa, ikiwa ni utekelezaji wa Maagizo ya ziara yake iliyofanyika tarehe 20 mwezi wa Desemba mwaka jana, Luhaga Mpina, amesema kuwa ujenzi huo holela, umekiuka Sheria ya Mazingira ya mwaka 2004 na kanuni zake na kumtaka mmiliki wa Kampuni hiyo kubomoa ukuta huo ndani ya siku thelathini na kinyume na hapo Serikali kupitia halmashauri ya wilaya ya Temeke na NEMC itabomoa ukuta huo kwa gharama za mmiliki wa kampuni hiyo.

Aidha,  Mpina ameitaka NEMC pamoja na Manispaa ya Temeke kuwasilisha kwake ndani ya siku tatu vibali vilivyomruhusu mmiliki mwingine wa kampuni ya KOBIL kujenga juu ya mtaro huo, kinyume na hapo hatua nyingine zitachukuliwa.

Kwa Upande wake Mkaguzi wa Wakala wa Barabara nchini TANROADS, Dismas Nyoni, amesema kuwa, TANROADS ina mpango wa muda mfupi wa kufanyia usafi mtaro huo ulioziba na kupita chini ya barabara katika eneo la Kilwa road, na kuzibua mtaro huo ili kuwapunguzia wananchi usumbufu katika msimu wa mvua zinazokuja.

Hata hivyo, Mpina ametemebelea Gereza la Keko kujionea utekelezaji wa maagizo yake ambapo awali gereza hilo lilikuwa likitiririsha maji taka katika maeneo ya makazi na kwa hivi sasa gereza la keko limekamilisha ujenzi wa miundombinu ya maji taka kwa asilimia 80.

 

 

 

Kamanda Sirro aeleza kinachomsibu Manji baada ya kubainika hutumia Dawa za kulevya
Video: Majaliwa asisitiza vita madawa ya kulevya