Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), kimesema kuwa haki ya kujieleza na kukusanyika iko shakani, kutokana na kuwapo kwa udhaifu katika sheria mbalimbali.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa Utetezi na Maboresho wa LHRC, Ana Henga wakati wa uzinduzi wa Kampeni ya Kulinda Uhuru wa Kujieleza na kukusanyika, amesema kuwa uhuru wa kujieleza ni mhimu kwani unaweza kulitoa taifa kutoka hapa lilipo na kuliwezesha kusonga mbele.
Aidha, Kampeni hiyo imeandaliwa na kituo hicho kupitia mradi wa uhakiki kwa kushirikiana na wadau washirika ambao ni jukwaa la wahariri Tanzania (TEF), Baraza la Habari (MCT), Policy Forum, Twaweza, Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP), Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD), Shirika la Wanawake katika Sheria na Maendeleo Afrika (WiLDAF) na Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora.
“Watu wengi wanaogopa kujieleza, vyombo vya Habari vinafungiwa kwa ujumla hali sio nzuri, uhuru wa kukusanyoika na kujieleza uko katika hatihati,”amesema Henga.
Hata hivyo amesema kuwa wameamua kufanya Kampeni hiyo baada ya kubaini changamoto kadhaa zinazofifisha uhuru wa kukusanyika.