Mabingwa wa kombe la shirikisho barani Afrika (CAF), TP Mazembe wapo katika harakati za kumsajili aliyekua beki wa kati wa timu ya taifa ya Ubelgiji Anthony Vanden Borre.
Beki huyo mwenye umri wa miaka 29, ni mzaliwa wa Jamuhuri ya kidemokrasia ya Kongo na mama yake mzazi ni raia wa nchi hiyo. TP Mazembe wanatarajia kukamilisha mpango wa usajili wa Vanden Borre ndani ya juma hili.
Hata hivyo maamuzi ya usajili wa Vanden Borre, yanasitisha mpango wa kustaafu soka alioutangaza Januari 10 mwaka huu, na atakua anarejea uwanjani kwa mara nyingine akiwa barani Afrika.
Vanden Borre aliwahi kucheza katika klabu za Montpelier (Ufaransa), Anderlecht (Ubelgiji), Portsmouth (England) Fiorentina na Genoa (Italia).
Vanden Borre ana uraia wa wa Ubelgiji na DRC na alichagua kulitumikia taifa hilo la barani Ulaya, akiwa na umri wa miaka 16.
Wakati wa fainali za kombe la dunia mwaka 2014, alicheza mchezo mmoja kati ya Ubelgiji dhidi ya Korea Kusini.