Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema Serikali ya awamu ya tano imedhamiria kumaliza migogoro yote inayowakabili wananchi katika maeneo mbalimbali nchini ukiwemo wa Loliondo uliodumu kwa miaka 25.

Majaliwa amesema hayo wakati akipokea taarifa ya Kamati Teule ya Kushughulikia Mgogoro wa Loliondo na kuahidi kuifanyia kazi pamoja na mawaziri husika.

Majaliwa aliunda kamati hiyo Disemba 2016 mara baada ya kumaliza ziara ya kikazi mkoani Arusha, na Machi 2, 2017 ameitisha kikao ofisini kwake mjini Dodoma ili kupokea taarifa ya Kamati hiyo.

Kiini cha mgogoro huo kimetajwa kuwa ni eneo la pori tengefu la Loliondo ambalo linagombewa na wawekezaji, wakulima, wawindaji kwa sababu ni mapitio ya wanyama, chanzo cha maji, mazalia ya wanyama, malisho ya mifugo na makazi.

Kamati hiyo inayoongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo ilikuwa na jukumu la kufanya mapitio ya nini kinachosababisha kuwepo kwa migongano katika eneo hilo ili Serikali itoe uamuzi wenye tija.

“Hatuwezi kuwa tunagombana miaka na miaka bila ya kuwa na solution, hilo hatuwezi kuendelea nalo lazima tushirikiane kumaliza migogoro. Nataka nchi nzima iwe na amani na utulivu,“ amesema.

Majaliwa amesema Serikali imedhamiria kumaliza migogoro hiyo ili kutoa fursa kwa wananchi kuendelea kushiriki shughuli nyingine za maendeleo.

“Wananchi ndio tegemeo letu na tunataka kuona wakinufaika na Serikali yao.Na Serikali haiko tayari kuona migogoro hiyo ikiendelea. Natumaini timu hii itatuwezesha kumaliza mgogoro huu,“ amesema.

Aidha, Majaliwa amewataka wadau wote katika maeneo mbalimbali nchini wahakikishe wanadumisha amani na washirikiane vizuri na Serikali na inapotokea dosari wasiingize ushabiki usiokuwa na tija.

 

Vissel Kobe Kumsajili Lukas Podolski
TP Mazembe Kumsajili Anthony Vanden Borre