Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imekubali ombi la Serikali ya Kenya la kuwapatia madaktari 500 kufuatia upungufu wa madaktari uliotokana na mgomo nchini humo.
Hayo yamesemwa leo Jijini Dar es salaam na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu alipokuwa akiongea na waandishi wa habari.
Amesema kuwa kutoka na maombi yaliyotolewa, Serikali imeandaa utaratibu kwa madaktari wa kitanzania kuwasilisha maombi yao katika tovuti ya wizara ya afya pamoja kufuata taratibu zingine kama watakavyoelekezwa.
Ummy Mwalimu amezitaja sifa za anayetakiwa kuomba nafasi hiyo kuwa ni shahada ya kwanza ya udaktari, mafunzo ya vitendo pamoja na kusajiliwa na Baraza la madaktari la Tanganyika na kutuma maombi hayo katika barua pepe; maombiyakazi@moh.go.tz kabla ya Machi 27 saa 10 jioni.
Aidha, ameongeza kuwa waombaji wanatakiwa kuambatanisha wasifu wao, nakala za vyeti vya taaluma na matokeo, cheti cha kuzaliwa, cheti cha kuhitimu mafunzo kwa vitendo pamoja na cheti cha usajili kutoka Baraza madaktari la Tanganyika.
“Tanzania hatuna upungufu wa madaktari isipokuwa Serikali haina uwezo wa kuajiri madaktari wote wanaohitimu, kwa kuwa kwa mwaka kuna wahitimu 1200 wa shahada ya kwanza ya udaktari na uwezo wa kuajiri ni 450 tu” amesema Ummy
Hata hivyo, Waziri Ummy amesema kuwa ajira hizo hazitawahusu watumishi wa umma, hospitali teule za halmashauri na mashirika ya hiari ambao wanalipwa mshahara na Serikali. Madaktari watakaokidhi vigezo na sifa watapewa mkataba wa ajira wa miaka miwili.
Nchi ya Kenya inakabiliwa na upungufu wa madaktari kutokana na mgomo ulioanza mwezi Desemba mwaka jana, ambapo madaktari hao wamekuwa wakaidai nyongeza ya mshahara na marupurupu mengine.