Serikali imewataka Maafisa Mawasiliano kuendelea kuitendea haki taaluma yao kwa kuhabarisha na kuisemea Serikali juu ya utoaji huduma za jamii na utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo.

Hayo yamebainishwa na Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Prof. Elisante Ole Gabriel wakati wa kufunga Kikao Kazi cha mwaka cha Maafisa Mawasiliano Serikalini mjini Dodoma.

“Mtaheshimika kwa kuiambia jamii na kuwapa taarifa kwa wakati. Nguvu ya habari ni kubwa, muitumie vizuri kwa kuongeza thamani ya kazi zenu na wafikisheni viongozi wenu kwenye mafanikio ya malengo yaliyowekwa. amesema Prof. Ole Gabriel.

Aidha, Ole Gabriel amewahimiza Maafisa hao kushirikiana na vyombo vya habari katika kutoa habari kwa manufaa ya Watanzania kwa kuzingatia Sheria za nchi ikiwemo Sheria ya Huduma za Habari ya mwaka 2016 na kanuni zake.

Katika hatua nyingine, Mkurugenzi wa Idara ya Habari (MAELEZO) ambaye pia ni Msemaji Mkuu wa Serikali Dkt. Hassan Abbasi amesema kuwa ili Vitengo vya Mawasiliano Serikalini viweze kuhabarisha Umma kwa wakati ni lazima kuwe na mawasiliano ya kimkakati ambayo yatasaidia kuisemea Serikali kwa wananchi wake katika mambo mbalimbali yanayotekelezwa na Serikali yao.

Hata hivyo, Mwenyekiti wa Chama cha Maafisa Mawasiliano ya Serikalini (TAGCO) Paschal Shelutete amemuahidi Mgeni Rasmi kwa niaba ya Washiriki wa Mkutano huo kuwa watayafanyia kazi maagizo yaliyotolewa pamoja na maazimio yaliyofikiwa katika mkutano huo  na kufanya kazi kwa weledi na kwa wakati ili kuhakikisha kazi za Serikali zinafahamika kwa Umma wa Watanzania.

Madaktari 500 kutoka Tanzania kuokoa jahazi nchini Kenya
Wanaume watelekeza familia zao