Katika hali ya kushangaza iliyoibuka hivi karibuni, Wanaume katika Wilaya ya Bariadi Mkoani Simiyu wanadaiwa kutelekeza familia zao pindi wake zao wanapojifungua watoto wenye ulemavu wa ngozi (Albino) kwa kile kinachaodaiwa kuwa ni imani potofu.

Aidha, baadhi ya wanawake ambao wamekimbiwa na wanaume, wamekuwa wakiwafungia ndani na kutowapeleka shuleni watoto wenye ulemavu huo wa ngozi kutokana na hofu ya kufanyiwa ukatili.

Hayo yamesemwa na Ofisa Ustawi wa Jamii Wilayani humo, Gigwa Masanja wakati akizungumza na wananchi wa Dutwa katika utekelezaji mradi wa mauaji, unyanyapaa na unyanyasaji kwa watu wenye ulemavu wa ngozi.

Mradi huo unatekelezwa na Shirika la Community Development Suppot (CDS) kutoka wilayani Meatu chini ya ufadhili wa The Foundation For Civil Sociaty.

“Tumekutana na matukio haya kwa kiwango kikubwa, mwanaume akiona mke wake amejifungua albino, anaamua kukimbia familia yake kwa imani hizo potofu, asilimia zaidi ya 60 katika Wilaya hii hawajapelekwa shule,”amesema Gigwa.

Kwa upande wake Mratibu wa Mradi huo wa CDS, Ester Joseph amesema kuwa shirika linatekeza mradi huo kwa miezi 6 katika Wilaya za Meatu, Itilima, pamoja na Bariadi.

Hata hivyo, baadhi ya wananchi wamesema kuwa pamoja na kupatiwa elimu hiyo bado vitendo hivyo vya unyanyasaji kwa watu wenye ulemavu wa ngozi bado vinaendelea.

 

Maofisa Mawasiliano Serikalini watakiwa kuitendea haki taaluma
Lowassa atoa ya moyoni kuhusu zuio la wabunge wa CCM