Mwanasiasa Mkongwe hapa nchini na Muasisi wa Chama cha Mapinduzi aliyeamua kukihama chama hicho kwa madai ya kutotenda haki katika mchakato wa kumpata mgombea urais wa chama mwaka 2015, Kingunge Ngombale Mwiru amesema kuwa bado kuna vigogo watatu wanaotakiwa kuadhibiwa ndani ya chama hicho kwakuwa wao ndio waliosababisha mambo yote yaliyotokea.
Kingunge ameyasema hayo alipokuwa akifanya mahojiano na MTANZANIA Jumapili, amewataja viongozi hao wa juu wanaopaswa kuadhibiwa kwa usaliti kuwa ni Mwenyekiti Mstaafu, Jakaya Kikwete, Makamu Mwenyekiti Bara, Philip Mangula na Katibu Mkuu Abdulrahman Kinana.
Aidha, kuhusu kilichotokea ndani ya CCM, kufukuzwa kwa baadhi ya Makada wa Chama hicho kwa tuhuma za usaliti, Kingunge amesema kuwa kitu hicho si kigeni kwani ni mwendelezo wa makosa yaliyojitokeza kwenye mchakato wa kumpata mgombea urais wa mwaka 2015.
“Sophia Simba alimsaliti nani? Madabida kamsaliti nani? na katika ngazi gani? ndiyo maana nasema hili lote ni mwendelezo wa yaliyotokea 2015 kule Dodoma,”amesema Kingunge.
Hata hivyo, Mwanasiasa huyo Mkongwe hapa nchini amesema kuwa anastaajabu sana kuona baadhi ya wanachama wanafukuzwa na wengine kupewa onyo kali kwa kile kinachoitwa usaliti, kwani wahusika wakubwa wa usaliti bado wamo ndani ya chama hicho na hawajaguswa na adhabu.