Mlinda mlango kutoka nchini Ufaransa Hugo Lloris ameutega uongozi wa Tottenham Hotspurs kwa kusema atasalia klabuni hapo, endapo meneja Mauricio Pochettino ataendelea kuwa bosi wake.
Lloris ametoa sharti hilo, kufuatia tetesi zinazoendelea kuhusu mustakabali wa Mauricio Pochettino ambaye ameanzwa kutajwa huenda akachukua nafasi ya ukuu wa benchi la FC Barcelona badala ya Luis Enrique atakaeondoka mwishoni mwa msimu huu.
Lloris amesema mpango wake wa kusaini mkataba mpya utategemea uwepo wa meneja huyo kutoka nchini Argentina, ambaye anamuamini na kuuthamini mchango wake tangu alipojiunga na Spurs mwaka 2014 akitoka Southampton.
“Uhusiano wetu umeendelea kuimarika siku hadi siku, sitokua tayari kufanya kazi na meneja mwingine endapo Mauricio Pochettino ataondoka na kutimkia kwingine.
“Naamini hata kwa wachezaji wenzangu wanatambua umahiri ya Mauricio Pochettino, amekua na ukaribu na kila mmoja, na ndio maana tunazingatia mafundisho yake wakati wote na kufikia hatua ya kupata matokeo mazuri uwanjani.
“Kama ataondoka hapa, litakua pigo kubwa sana kwa Spurs, kuna haja kwa viongozi kupambana kadri wawezavyo ili kuziba mianya ambayo huenda ikamuwezesha kutimkia huko ambapo anatajwa.” Alisema Lloris
Kauli hiyo ya Lloris huenda ikawa faraja kwa viongozi wa Paris Saint-Germain na Real Madrid ambao kwa pamoja wameshatangaza hadharani kumuwania mlinda mlango huyo.