Beki wa klabu ya AS Roma Antonio Rudiger huenda akatua magharibi mwa jijini London yalipo maskani ya vinara wa ligi ya nchini England (Chelsea) utakapowadia wakati wa usajili wa majira ya kiangazi.

The Blues wamemfuatilia beki huyo kwa kipindi kirefu na wamejiridhisha ana uwezo wa kuwa sehemu ya kikosi chao, ili kuboresha safu ya ulinzi msimu ujao wa 2017/18.

Sun Sports wameripoti kuwa, Chelsea wametenga kiasi cha Pauni milioni 30, kwa ajili ya usajili wa beki huyo mwenye umri wa miaka 24, huku wakitambua huenda wakapata upinzani mkubwa kutoka kwenye klabu nyingine za barani Ulaya.

Klabu za mjini Manchester (Man Utd na Man City) zote zinatajwa kuwa katika mawindo ya kumuwania beki huyo kutoka nchini Ujerumani, lakini bado uchunguzi uliofanywa na Sun Sports umebaini Chelsea wana nafasi kubwa ya kushinda vita hiyo.

Hata hivyo uongozi wa AS Roma, umeonyesha kuwa tayari kufanya biashara ya kumuachia Rudiger, kwa sharti la kupewa pesa sambamba na kumsajili kiungo kutoka nchini Hispania Cesc Fabregas.

Endapo dili hilo litafanyika, Rudiger anapewa nafasi kubwa ya kutengeneza ukuta wa Chelsea kwa kushirikiana na Gary Cahill ambaye usiku wa kuamkia leo, alikiongoza kikosi cha England katika mpambano wa kimataifa wa kirafiki dhidi ya Ujerumani mjini Dortmund.

Joe Hart Kuondoka Jumla Man City
Hugo Lloris Atikisa Kibiriti White Hart Lane