Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa amesema kuwa sera ya uwekezaji nchini inasema mitambo wa kutenganisha madini ya dhahabu na shaba inatakiwa uwepo nchini ili kila hatua ya uchenjuaji ifanyike hapa hapa.
Amesema miongoni mwa masharti ya uwekezaji kwenye sekta ya madini nchini ni kwamba mitambo hiyo ije kujengwa hapa nchini, pia iongeza fursa ya ajira na kukuza sekta nyingine ikiwemo ya kilimo.
Majaliwa amesema hayo Machi 27, 2017 alipo fanya ziara kwenye mgodi wa dhahabu wa Buzwagi uliopo wilaya ya Kahama mkoani Shinyanga, ambapo amechukua sampuli za mchanga katika makontena mbalimbali kwa lengo la kwenda kuyapima kwa wataalamu wa madini ili kubaini kiasi cha dhahabu kilichomo.
Amesema wanataka kuona mchanga unaosafirishwa na mwekezaji huyo unakiasi gani cha dhahabu, pia Serikali inataka kufahamu kama kodi inayolipwa ni sahihi.
” Hata hivyo tayari Mheshimiwa Rais Dkt. John Magufuli alishatoa tangazo la kuzuia usafirishaji wa michanga kwenda nje ya nchi,”.
“Tumeamua kuchukua sampuli za mchanga ambao mwekezaj anasema wanaupeleka nje ya nchi kwa ajili ya kwenda kutenganisha madini ya dhahabu na shaba. Hata hivyo nimemuhoji kwa nini mitambo hiyo isiletwe nchini ili kila kitu kifanyike hapahapa,” amesema Majaliwa
Aidha, Majaliwa amewataka Watanzania kuwa nasubira wakati Serikali ikiendelea na zoezi la kuchunguza athari zitokanazo na kusafirisha mchanga wa madini nje ya nchi. Pia amewatoa wasiwasi wafanyakazi katika migodi na wamiliki kutowapunguza na badala yake waache waendelee na majukumu yao.
Naye Meneja Uendelezaji wa mgodi huo, George Mkanza amesema mgodi huo ulionzishwa mwaka 2009 umeajiri watumishi 720 pamoja na vibarua 500.
Mkanza amesema kwa siku wanachenjua makontena matatu hadi sita ambapo katika kila kontena moja wanapata kilo tatu za madini ya dhahabu na tani nne za madini ya shaba. Wanazalisha asilimia 50 ya madini ya dhahabu na asilimia 50 ya dhahabu iko kwenye mchanga na inakuwa imechanganyika na madini ya shaba ambayo ndiyo unaosafirishwa kwenda nje ya nchi kwa ajili ya kutenganishwa.
Amesema kuwa mgodini hapo kuna makontena 179, makontena mengine 152 yako Dar es Salaam kwenye bandari kavu ya Nazam na 21 yako bandarini.
“Kila siku tunapoendelea kuzalisha tunakuwa na makontena manne hadi sita. Ndugu zetu wa Bulyanhulu nao wanamakontena 108 yako mgodini na 104 yako Nazam Cargo Dar es Salaam,” alisema.