Aliyekuwa muuguzi wa Hosptali ya Mkoa wa Mara, Irene Machagge amehukumiwa kifungo cha miaka mitatu jela au kulipa faini ya shilingi laki sita baada ya kukutwa na hatia ya kugushi cheti cha elimu ya sekondari.
Akisoma hukumu hiyo, Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Mara, Karim Mush alisema kuwa mahakama hiyo imefikia uamuzi huo baada ya kujiridhisha pasipo na shaka yoyote kuwa ushahidi uliotolewa na upande wa mashtaka ulikuwa sahihi.
Machagge alifikishwa katika mahakama hiyo kwa mara ya kwanza Novemba mwaka 2015, akishtakiwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kwa madai kughushi cheti cha elimu ya sekondari cha shule ya Sekondari ya Forodhani, ambacho alikiwasilisha kwa Katibu Tawala wa mkoa wa Mara mwaka 2009 na kukitumia kujipatia ajira ya uuguzi.
Katika utetezi wake, mshatakiwa aliiomba mahakama kumpunguzia kifungo kwani ana ujauzito na pia anasumbuliwa na ugonjwa ambao hamruhusu kukaa katika sehemu yenye joto.
Akitoa mchanganuo wa hukumu hiyo, Hakimu Mush alieleza kuwa mshatakiwa anatakiwa kutoa faini ya shilingi 500,000 kwa kosa la kughushi cheti na shilingi 100,000 kwa kosa la kukitumia kujipatia ajira, au kwenda jela kwa makosa yote mawili.
Mshtakiwa alitoa faini hiyo kwa mkupuo, hivyo hakwenda jela