Klabu ya Azam itaendelea kumkosa nahodha na mshambuliaji wake tegemeo, John Bocco katika michezo minne mfululizo.
Daktari wa klabu hiyo, Mwanandi Mwankemwa, alisema kuwa Bocco bado ni mgonjwa na atakuwa tayari kuanza mazoezi ifikapo Aprili 15 mwaka huu.
Mwankemwa alisema kutokana na hali yake kutoimarika, Bocco hataweza kuitumikia timu yake katika michezo mitatu ya Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Yanga, Mtibwa Sugar na Ruvu Shooting.
“Pia Bocco hataweza kucheza katika mechi ya hatua ya robo fainali ya mashindano ya Kombe la FA dhidi ya Ndanda FC iliyopangwa kufanyika Aprili 5 kwenye Uwanja wetu wa Azam Complex,”, alisema Mwankemwa.
Wakati huo huo, daktari huyo amependekeza mchezaji wa kimataifa wa timu hiyo Stephano Kingue, kupelekwa nje ya nchi kupata matibabu zaidi.
Kikosi cha Azam ambao ni mabingwa watetezi wa Kombe la Kagame kinajiandaa kuwakabili Yanga katika mechi ya Ligi Kuu Bara itakayofanyika kesho kwenye Uwanja wa Taifa na matokeo yake yataonyesha mbio za ubingwa zinavyokwenda.
Simba ndiyo vinara katika msimamo wa ligi hiyo na endapo Yanga itafungwa au itatoka sare na wao kushinda Jumapili dhidi ya Kagera Sugar, watakuwa wamejiweka kwenye mazingira mazuri.