Rais wa Marekani, Donald Trump amesema kuwa nchi yake italitatua suala la vitisho vya silaha za nyuklia kutoka Korea Kaskazini hata bila msaada wa China.
Trump ameyasema hayo katika mahojiano aliyofanya na UK paper wikendi iliyopita akisisitiza kuwa Marekani ina uwezo huo kwa kiwango chote.
“Kama China haitalitatua suala la Korea Kaskazini, sisi tutafanya hivyo wenyewe. Hicho ndio kitu ambacho naweza kukwambia,” Rais Trump anakaririwa.
Alieleza kuwa anafahamu China ina nafasi kubwa ya kulitatua suala la vitisho vya silaha za kinyuklia vinavyotolewa na Korea Kaskazini, lakini inao uhuru wa kuamua kusaidia ama kuachana nalo, lakini Marekani haitashindwa kulikabili.
“China ina ushawishi mkubwa juu ya Korea Kaskazini. Na China itaamua kutusaidia au kutotusaidia kulishughulikia suala la Korea Kaskazini. Kama watatusaidia itakuwa vema kwao, na kama hawatasaidia haitakuwa vema kwa wote,” alisema Rais huyo wa Taifa lenye nguvu kubwa zaidi duniani bila kutoa maelezo ya hatua atakazochukua.
Msimamo huo wa Trump umekuja ikiwa tayari kuna ratiba ya kukutana na Rais wa China, Xi Jinping, wiki hii.