Shirika la Mkulima Market linatarajia kufanya soko la wazi (Mkulima soko) Jijini Dar es Salaam katika viwanja vya Chuo Kikuu cha Dar es salaam (UDSM) Aprili 12 mpaka 15 mwaka huu.
Hayo yamesemwa na Mratibu wa Mkulima Market, Vicensia Shule wakati akiongea na waandishi wa habari kuhusu soko hilo la wazi mapema hii leo jijini Dar es salaam.
Amesema kuwa, maonyesho hayo yatahusisha mauzo ya bidhaa mbalimbali za kilimo, uvuvi na ufugaji na amewakaribisha wadau mbalimbali kutoka katika taasisi za umma, sekta binafsi, wafanyabiashara na makundi mbalimbali kushiriki kuuza, kuonyesha, kutoa huduma na elimu kuhusu ukulima.
Nae, Mratibu Msaidizi wa shirika hilo, Vicent Mirumbe ametoa wito kwa vijana kushiriki maonyesho hayo ambayo yatawasaidia kuwainua kiuchumi na kutowategemea wazazi au walezi.
Hata hivyo, Mkulima Market pia imeandaa masoko mengine ya wazi katika kipindi cha sikukuu kubwa tatu ambazo ni Eid al Fitr Juni 21 hadi 24 mwaka huu, Eid al Hadj Agosti 29 hadi Septemba 1 mwaka huu na Krismasi Desemba 20 hadi 24 mwaka huu, ambapo katika soko la wazi la Desemba kutakua na Tamasha la Maembe (Mango Festival)