Siku moja baada ya wabunge wanaoiunga mkono kambi ya Katibu Mkuu wa Chama Cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad kutangaza mpango wa kwenda kufanya usafi katika Ofisi za Makao Makuu ya chama hicho, Buguruni jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti anayetambuliwa na Ofisi ya Msajili wa vyama vya siasa, Profesa Lipumba ametoa msimamo wake.
Profesa Lipumba aliingia na kuendelea kufanya kazi katika ofisi za Makao Makuu ya chama hicho baada ya kupata barua ya kutambuliwa na Msajili kama mwenyekiti halali. Tangu wakati huo Maalim Seif na wafuasi wake hawakuwahi kuingia ofisini hapo.
Jana, Mbunge wa Temeke, Abdallah Mtolea alitangaza kuwa wabunge wa CUF pamoja na wafuasi wao wataenda kufanya usafi katika ofisi hizo na kwamba watasafisha kila ambacho sio halali.
“Wanachama wa CUF ambao hawakubali Profesa Lipumba kuwa Mwenyekiti, wameamua kwenda kufanya usafi kwenye ofisi zao za Buguruni,” alisema Mtolea.
“Na hatua hii imekuja baada ya kuona ofisi ile inatumika vibaya. Imekuwa ndio kijiwe cha wahundi kupanga matukio ya kihalifu kama kuvamia mikutano ya waandishi wa habari,” aliongeza mbunge huyo anayemuunga mkono Maalim Seif.
Akijibu kuhusu hatua hiyo, Profesa Lipumba amesema kuwa wabunge hao hawana nia ya kufanya usafi katika ofisi hizo bali wanataka kufanya vurugu na kwamba tayari amesharipoti polisi.
“Wanataka kuleta vurugu ili CUF ionekane ina taswira mbaya kwa Watanzania. Naomba wanachama waepuke mtego huu, namshauri (Mbunge wa Temeke, Mtolea) akafanye usafi huo Temeke, mbona kuna masoko mengi tu machafu,” Profesa Lipumba anakaririwa na Mwananchi.
Kwa upande wa Mtolea, alisisitiza kuwa wanakwenda kwenye Makao Makuu ya ofisi zao hivyo hawahitaji kuomba ruhusa.