Maandamano ya maelfu ya wananchi nchini Venezuela yaliyopelekea mitaa kufurika, yamesababisha ongezeko la vifo leo hadi kufikia watu 30.
Maandamano hayo yaliyoanza majuma kadhaa yaliyopita, yameshuhudia maelfu ya wananchi wakiwa mtaani na mabango wakipinga hatua ya Serikali ya Rais Nicolas Maduro kuanza mchakato wa kufanya mabadiliko kwenye katiba ya nchi hiyo.
Shirika la habari la ‘Associated Press’ limeripoti kuwa waandamanaji wamekuwa wakikabiliana na jeshi la Polisi katika mji mkuu wa Caracas, ambapo imeshudiwa baadhi yao wakichoma magari na kufanya uharibifu mkubwa wa mali. Polisi wamefyatua mabomu ya machozi kuwazuia waandamanaji kutoendelea na safari yao ya kuelekea kwenye Bunge la nchi hiyo.
Saa chache zilizopita, ilisambaa picha inayoonesha tukio la kusikitisha ambapo mmoja kati ya waandamanaji aliungua vibaya kwa moto baada ya tanki la mafuta ya gari la polisi kulipuka.
Rais Maduro amewalaumu wapinzani wake kisiasa kuwa wanashirikiana na nchi za magharibi kuhamasisha maandamano hayo kwa lengo la kuvuruga sera zake za ujamaa, na kusisitiza kuwa kamwe hatavumilia vurugu na machafuko yanayofanyika.
Umoja wa Mataifa umeitaka Serikali ya Venezuela kuwaruhusu wananchi kuandamana kwa amani.
“Tusikitishwa sana na madai ya matumizi ya nguvu kupita kiasi dhidi ya waandamanaji, pamoja na vifungo na mauaji yanayowakabili,” Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa limesema katika tamko lake.