Katibu Mkuu wa Chama Cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad amesema kuwa yuko tayari kujiuzulu nafasi yake na kuweka kando siasa endapo wananchi watamtaka kufanya hivyo.

Mwanasiasa huyo mkongwe aliyewahi kushika nyadhifa za juu kwenye Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, aliyasema hayo jana katika mahojiano maalum na kipindi cha Clouds 360, cha Clouds TV kilichorushwa pia kupitia Clouds FM.

“Suala la kujiuzulu sio jambo la ajabu. Mimi najua napendwa na wananchi tena napendwa kweli. Jambo moja kuwa iwapo [wananchi] wakisema sasa inatosha niondoke nitafanya hivyo,” anakaririwa.

Maalim ambaye amekwishagombea nafasi ya urais wa Zanzibar mara tano bila mafanikio, ameanza ziara yake jijini Dar es Salaam kwa lengo la kukijenga chama chake ambacho kiko katika mgogoro mkubwa.

Katika hatua nyingine, Maalim aliweka wazi msimamo wake kuwa kamwe hatafanya mazungumzo na Mwenyekiti wa chama hicho anayetambuliwa na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, Profesa Ibrahim Lipumba.

Alisisitiza kuwa kukaa meza moja na Profesa Lipumba ambaye alidai ni msaliti ni bora akae na CCM ambao ni mahasimu wake kwani atachukua tahadhari.

Akizungumzia uwepo wa Profesa Lipumba katika ofisi za makao makuu ya chama hicho zilizoko Buguruni, alisema kuwa hayuko pale kihalali kwani aliingia kwa kuvunja milango na kuwapiga walinzi kinyume cha sheria. Alisisitiza kuwa Lipumba sio tu kwamba hawamtambui kama Mwenyekiti wa chama, bali pia sio mwanachama wa chama hicho baada ya kuvuliwa uwanachama na Baraza Kuu.

Vifo Vyaongezeka Maandamano Kupinga Maamuzi ya Serikali Venezuela
Video: Lipumba anena mazito kuhusu Maalim, amtaka aache usultani