Wakili maarufu anayetajwa kuwa mtetezi wa haki za binadamu nchini Thailand, Prawet Prapanukul anakabiliwa na kifungo cha hadi miaka 150 jela kwa tuhuma za kumkashfu mfalme.
Wakili huyo ambaye alikuwa akitoa huduma za kisheria kwa wajumbe wa chama cha upinzani cha United Front for Democracy, anakabiliwa na mashtaka 10 ya kumkashfu mfalme na familia yake na endapo atakutwa na hatia, atatumikia kifungo hicho kwa mujibu wa sheria za nchi hiyo.
Prapanukul mwenye umri wa miaka 57, alikamatwa wikendi iliyopita alipokuwa anarejea nyumbani kwake, na jana alifikishwa mahakamani kuanza kujibu tuhuma zinazomkabili.
“Anakabiliwa na makosa 10 ya kukiuka ibara ya 112 ya sheria, kwahiyo inaweza kumfanya afungwe miaka hadi 150 endapo atakutwa na hatia.,” Chama cha Mawakili cha Thailand cha kutetea haki za binadamu kililiambia shirika la habari la Reuters.
Chama hicho kiliongeza kuwa mbali na makosa hayo, Prapanukul pia anakabiliwa na mashtaka mengine matatu tofauti ya kuvunja ibara ya 116 ambayo yanaweza kumfanya ahukumiwe kifungo cha miaka saba jela kwa kila kosa.