Tanzania ni nchi pekee Barani Afrika kuwa na taasisi inayojihusisha na masuala ya Kemikali ambayo ipo chini ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto.
Hayo yamsemwa na Mkemia Mkuu wa Serikali, Prof. Samweli Manyele alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es salaam kuhusu mkutano wa Kimataifa wa Udhibiti Kemikali na Kemikali taka uliofanyika Geneve, Uswisi kuanzia April 24 hadi Mei 5 mwaka huu.
Amesema kuwa kuwa Tanzania inashikilia nafasi ya tatu kwakuwa na sheria bora ya usimamizi na Udhibiti wa Kemikali Barani Afrika huku ikitanguliwa na nchi za Afrika Kusini na Nigeria.
“Taasisi yenye kusimamiwa na wataalamu wa kemikali waliobobea pamoja na kuwa na maabara kubwa inayojulikana kimataifa, Tanzania ni pekee hivyo tumedhuria ule mkutano tukiwa na mchango mkubwa katika sekta hiyo,” amesema Prof. Manyele.
Ameongeza kuwa kushiriki katika mkutano huo ni jambo la kisheria hivyo kupeleka watumishi watatu kutoka kwenye taasisi hiyo inadhihirisha kuwa Tanzania imetimiza majukumu yake kama Taifa.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi Idara ya Huduma ya Ubora wa Bidhaa, Daniel Ndiyo ametaja wadau wanaotakiwa kupata taarifa na maamuzi ya mkutano huo kuwa ni wafanyabiashara, watumiaji wa kemikali hizo pamoja na mamlaka mbali mbali za usimamizi wa kemikali.
Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali ilishiriki katika mkutano huo wa utekelezaji wa mikataba mitatu ikiwemo ya usafirishaji wa taka sumu kimataifa (Basel), mkataba unaohusu kemikali zenye madhara na zinazochukua muda mrefu kuoza katika mazingira (Stockholm) pamoja na mkataba wa Rotterdam unaohusu upashanaji taarifa juu ya kemikali hatari na viuatilifu katika biashara ya kimataifa.