Mashindano ya ngumi yaliyoandaliwa na Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Isaya Mwita yamemalizika huku Timu ya JKT Makao Makuu ikiibuka mabingwa wa kombe hilo ikiwa ni kwa Mara ya nne mfululizo.
JKT imeibuka mshindi wa mashindano hayo kufuatia wachezaji wake kupata medali nne za dhahabu, huku Timu ya Magereza ikipata medali mbili, Kigamboni medali moja na Mombasa medali moja.
Akizungumza mara baada ya kutoa zawadi kwa washindi, Mbunge wa Temeke, Abdallah Mtolea amempongeza Mstahiki Meya wa jiji kwa kuandaa mashindano hayo na kusema kuwa ni mchezo ambao una washabiki wengi na kwamba amewatendea haki wananchi wa jiji lake ambao wanapenda mchezo huo.
“Uwepo wa mashindano haya umewezesha kuwakutanisha vijana pamoja kutoka sehemu mbalimbali na hivyo itachangia zaidi katika uhamasishaji wa kujiepusha na matukio ya kiuhalifu, makundi mabaya kama vijana,”amesema Mtolea.