Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango leo Juni 8, 2017 amewasilisha Bungeni Bajeti ya mwaka wa fedha 2017/2018 ambapo katika hotuba yake amependekeza kufanya marekebisho katika sheria ya Fedha ya Serikali za Mitaa.
Dkt. Mpango amesema kuwa marekebisho hayo yanalenga kupunguza ushuru unaotozwa na Halmashauri za Wilaya kutoka kiwango cha sasa cha asilimia 5 ya thamani ya mauzo hadi asilimia 3 kwa mazao ya biashara na asilimia 2 kwa mazao ya chakula.
“Napendekeza kufanya marekebisho kwenye Sheria ya Fedha ya Serikali za Mitaa, Sura 290 ili kupunguza Ushuru wa Mazao (Produce Cess) unaotozwa na Halmashauri za Wilaya” – Amesema Dkt Mpango
Aidha, Dkt. Mpango amesema kuwa mtu anayesafirisha mazao yake kutoka Halmashauri moja kwenda nyingine yasiyozidi tani moja 1 asitozwe Ushuru.
Amesema kuwa lengo la hatua hiyo ni kuwawezesha wakulima kulipwa bei stahiki ya mazao yao na hivyo kuboresha mapato yao, ambapo ameeleza kuwa hatua hiyo inatarajiwa kuhamasisha uzalishaji wa mazao.