Aidha, Majaliwa amezungumzia hatua mbalimbali zinazochukuliwa na Serikali katika mapambano dhidi ya rushwa.
Amesema Serikali imeanza kupata mrejesho mzuri kwamba watumishi wa umma wanawajibika ipasavyo na vitendo vya rushwa vinaendelea kupungua.
“Baadhi ya hatua tulizochukua ni pamoja na kuimarisha taasisi yetu ya TAKUKURU; kuimarisha matumizi ya mashine za kielektroniki ili kupunguza mianya ya kupoteza mapato; kuanzisha mahakama ya mafisadi; kusimamia nidhamu katika utumishi wa umma na kuchukua hatua za haraka za kinidhamu na za kisheria dhidi ya watuhumiwa wote wa rushwa na ufisadi,” amesema.
Pia, Majaliwa amewaomba wabunge kuendelee kuiunga mkono Serikali kwani haina mzaha kwenye mapambano hayo.
“Serikali haina mzaha kwenye mapambano dhidi ya rushwa na tutaendelea na mapambano hayo. Hivyo, ninaomba waheshimiwa wabunge muendelee kutuunga mkono katika mapambano haya, twende kwa wananchi tukatoe wito kwao watuunge mkono kwenye vita hii,” amesisitiza.
“Tayari tumefanya tathmini na kubaini mianya ya rushwa katika sekta za ardhi, uchukuzi, biashara na maji na hivyo kuziba mianya hiyo. Tutaendelea kuiwezesha TAKUKURU ili iendelee na kazi nzuri waliyoianza ya kubaini mianya na kutoa ushauri wa kuziba mianya hiyo ya rushwa. Lengo letu ni kuwekeza zaidi kwenye kuzuia, kwa kuwa kinga ni bora kuliko tiba”.