Shirikikisho la Masumbwi Duniani (WBO) limekubali kufanya uamuzi mpya wa pambano la Manny Pacquiao na Jeff Horn baada ya kupokea barua rasmi kutoka kwa baraza la masumbwi la Ufilipino pamoja na malalamiko mengi kutoka kwa wadau wa masumbwi.
Horn alimvua Pacquiao mkanda wa ubingwa wa masumbwi uzito wa welterweight katika pambano lililofanyika nchini Australia, Julai 2 mwaka huu. Hata hivyo, matokeo yaliyotolewa na majaji watatu yalipingwa vikali na wadau wengi akiwemo bondia Manny Pacquiao punde alipowasili nchini kwake akifuta kauli ya awali ya kuyakubali.
WBO wameeleza kuwa watateua jopo la majaji watano wa kujitegemea ambao watatoa alama mpya kwa kila raundi ya pambano hilo kwa kuangalia mkanda wa video.
Hata hivyo, shirikisho hilo limeeleza kuwa hatua hiyo itakuwa kwa lengo la kuwaonesha mashabiki uhalisia lakini haitabadili matokeo ya pambano husika.
“Lengo la kufanya marejeo ni kuweza uwapa mashabiki mwanga wa nani alishinda kweli pambano hilo kwa uhalisia hata kama hatuna uwezo wa kubatilisha uamuzi wa awali wa majaji wa pambano hilo,” Rais wa WBO, Francisco Valcarcel aliiambia Associated Press.
Hata hivyo, wakati uamuzi huo unatolewa, tayari Horn na Pacquiao wameshakubaliana kushiriki pambano la marudiano mwaka huu.