Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) leo kimetangaza oparesheni yake mpya waliyoibatiza jina la ‘Ondoa Msaliti Buguruni’ ikimlenga mwenyekiti wa Chama Cha Wananchi (CUF) anayetambuliwa na ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, Profesa Ibrahim Lipumba.
Makamu mwenyekiti wa Chadema kanda ya Pwani ambaye pia ni Mbunge wa Ubungo, Saed Kubenea amesema kuwa wamefikia uamuzi huo baada ya kufanya vikao na viongozi wa CUF na kubaini kuwa mgogoro ndani ya chama hicho una athari kubwa kwa muungano wa vyama vya upinzani na kwamba unachochewa na chama tawala.
Kubenea ambaye ametangaza oparesheni hiyo leo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, amesema oparesheni hiyo imeanza rasmi leo na kwamba inataratibiwa na Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kwa ajili ya kumuunga mkono Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad.
Alisema lengo kuu ni kuhakikisha wanamuondoa Profesa Lipumba kwenye Ofisi za Makao Makuu ya CUF zilizoko Buguruni jijini humo, kwa madai kuwa ni msaliti.
“Sisi kama Chadema tumeamua kuwasaidia viongozi na wanachama wa CUF kumuondoa msaliti [Profesa] Lipumba Buguruni, kutupa nguo zake na viongozi halali wa CUF watarudi Buguruni,” Kubenea anakaririwa.
Hata hivyo, Profesa Lipumba ameendelea kusisitiza kuwa ndiye mwenyekiti halali wa CUF anayetambuliwa na ofisi ya msajili. Mwanasiasa huyo ambaye alitangaza kubatilisha uamuzi wake wa kujiuzulu nafasi ya uenyekiti wa chama hicho hali iliyozua sintofahamu, hivi karibuni alipata mafanikio zaidi baada ya ofisi ya msajili kuitambua bodi mpya ya wadhamini ya chama hicho ambayo inamuunga mkono.
Lipumba amekuwa akisisitiza kuwa anamsubiri Maalim Seif afike ofisini ili ampangie kazi na kwamba kwa sasa majukumu yake yanafanywa na Naibu Katibu Mkuu Bara, Magdalena Sakaya.