Aliyekuwa Msemaji wa Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Klabu ya Yanga, Jerry Muro amesema kuwa yeye alishakuwa maarufu kabla ya Yanga hivyo hakuwa katika Klabu hiyo kwaajili ya kutafuta umaarufu bali alikwenda kuiimarisha Klabu hiyo.
Ameyasema hayo jijini Dar es salaam alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari, ambapo amesema kuwa katika kipindi chake cha uongozi katika Klabu hiyo aliisaidia kupata mafanikio makubwa.
“Mimi kabla hata ya kwenda kuwa Msemaji wa Klabu ya Yanga nilikuwa tayari ni maarufu, hivyo nilienda kufanya kazi na wala huwezi kunifananisha na mtu yeyote wa kunilinganisha nae, hata kukosa nafasi ya kuendelea na kazi yangu wala haijaniuma chochote,”amesema Muro
Akizungumzia kuhusu msemaji mpya wa Klabu hiyo, amewataka wanachama wa Yanga kumpa muda ili aweze kuonyesha uwezo wake katika kutekeleza majukumu yake ambayo yanamkabili.
Hata hivyo, ameongeza kuwa anajivunia kazi yake aliyoifanya kwani kila sehemu aliyopita ameweza kupata mafanikio makubwa katika idara yake aliyokabidhiwa kuisimamia akiwa kama mkuu.