Wajumbe wa Bodi ya Skimu ya Umwagiliaji ya Mkula wamewekwa ndani mara baada ya kutolewa agizo na Mkuu wa Wilaya ya Kilombero, James Ihunyo baada ya kubainika kuchelewesha kwa makusudi malipo ya mkopo walioupata kutoka Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB).
Amesema kuwa uzembe wa Wajumbe wa Bodi hiyo umepelekea kuchelewesha marejesho ya mkopo huo wa takribani shilingi milioni 790 ambazo zilitakiwa kulipwa kwa muda muafaka..
“Lengo la mikopo hiyo ni kuinua ukuaji wa uchumi na kupunguza umaskini nchini Tanzania, hivyo kuchelewesha mikopo hiyo kwa makusudi ni kurudisha nyuma juhudi hizi,” amesema Ihunyo
Aidha, ameongeza kuwa kuchelewesha kurudisha mikopo hiyo kunakosesha wakulima wengine fursa ya kupata mikopo hiyo nafuu inayotolewa na TADB ambayo imelenga kuchagiza na kusaidia Mapinduzi ya Kilimo kutoka kilimo cha kujikimu kwenda cha kibiashara.
Kwa upande wake, Mwakilishi wa Mkurugenzi Mtendaji, Adam Kamanda amesema kuwa tangu wapatiwe mkopo huo, baadhi ya wakulima wa Skimu hiyo wamekuwa wakichelewesha kwa makusudi kurejesha mkopo huo licha ya jitahada za kuwahimiza kurejesha.