Serikali imewataka waendesha michezo ya kubahatisha na wadau waliokua wakilipa kodi kwenye Bodi ya Michezo Tanzania (Gaming board of Tanzania) kulipa kodi na mawasilisho ya makusanyo yao kwa Kamishna wa Kodi za Ndani wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).
Hayo yamesemwa mapema hii leo jijini Dar es salaam na Kamishna wa kodi za ndani, Elijah Mwandumbya alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari, mbapo amesema kuwa kufuatia mabadiliko ya Sheria ya Fedha namba 4 ya mwaka 2017 yaliyofanywa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwenye Sheria ya Michezo ya kubahatisha sura namba 166, TRA imepewa jukumu la kukadiria,kukusanya kodi kwenye michezo hiyo kuanzia Julai 1, mwaka huu.
Aidha, Mwandumbya amewataka walipaji kodi hao kuzingatia mambo mbalimbali ikiwa ni pamoja na kusajili biashara hizo ili kupatiwa namba ya mlipakodi (TIN) kwa wasiosajiliwa.
“Kwa waendesha biashara hiyo walioko jijini Dar es Salaam ambao walipata namba za utambulisho kwenye mikoa ya kikodi ya Ilala, Kinondoni na Temeke wanatakiwa kuwasilisha makusanyo yao kwenye ofisi ya TRA iliyopo Mtaa wa Lumumba, Kwa waliopo mikoa mingine watahudumiwa kwenye mikoa ya kodi walikopatia utambulisho wa mlipakodi,”amesema Mwandumbya
Naye Mkurugenzi wa Idara ya Elimu kwa Mlipa Kodi, Richard Kayombo amesema kuwa kodi hiyo kwa waendeshaji michezo ya kubahatisha sio kitu kipya ila kilichobadilika ni mahali pa kulipia.
Hata hivyo, Mamlaka ya mapato Tanzania imetoa wito kwa walipakodi wote kulipa kodi na kuwakilisha makusanyo yao kwa wakati ili kujiepusha na adhabu na gharama zisizo za lazima zitakazotokana kutokulipa kodi kwa wakati.