Serikali imepokea dola milioni 15 kutoka Taasisi ya Bill & Melinda Gates ili kusaidia mfumo wa kielektroniki ambao utaimarisha upatikanaji wa hudum bora katika sekta ya afya nchini.
Hayo yamesemwa mapema hii leo jijini Dar es salaam na Mwenyekiti mwenza wa Taasisi hiyo tajiri namba moja Duniani, Bill Gate katika uzinduzi wa mfumo huo uliofanyika katika ofisi ndogo za Wizara ya afya.
Amesema kuwa mfumo huo utasaidia kuimarisha na kuboresha matumizi sahihi ya takwimu na kuleta matokeo sahihi katika kufuatilia sawa pamoja na taarifa za utoaji wa chanjo.
”Mfumo huu utasaidia na kuleta ufanisi katika utekelezaji wa majukumu ,maamuzi kwa watendaji wa afya nchini Tanzania katika kutoa na kuboresha huduma kwa wananchi wao,” amesema Bill Gate.
Kwa upande wake Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii,Jinsia, Wazee na Watoto Ummy Mwalimu amesema kuwa Serikali ya awamu ya tano imekua ikitilia mkazo na matokeo ya chanjo katika kuleta ufanisi katika sekta ya afya.
Hata hivyo, ameongeza kuwa mfumo huo utaboresha upatikanaji na uhifadhi wa taarifa za wagonjwa kirahisi tofauti na zamani kwani mafaili mengi kwa sasa yanahifadhiwa kwa uhakika na usalama zaidi.