Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amempa siku 15 mweka hazina wa wilaya ya Sikonge, Evans Shemdoe ajieleze ni kwa nini ameshindwa kufikisha asilimia 80 ya makusanyo ya ndani.

Majaliwa ametoa agizo hilo leo Agosti 10, 2017 wakati akizungumza na watumishi na watendaji wa wilaya hiyo, mjini Sikonge.

“Nataka maelezo yakayoniridhisha ni kwa nini hamkufikisha asilimia 80 ya makusanyo ya halmashauri ambacho ni kiwango cha chini. Nzega TC wamefikisha asilimia 112, Kaliua wana asilimia 91, Nzega DC wana asilimia 80, ni kwa nini wewe umeshindwa kufikisha kiwango hicho?,” alihoji Waziri Mkuu.

“Ninataka nipate maelezo pia ni ipi mipango yenu ya kukusanya mapato kwa maeneo mliyoshindwa kufanya vizuri, na pia mmejipangaje kwa mwaka ujao wa fedha. Niyapate maelezo hayo ifikapo tarehe 25 Agosti,” amesema.

Akijieleza mbele ya Waziri Mkuu, mweka hazina huyo alisema wamefikisha asilimia 76.7 na wameshindwa kufikia lengo kwa sababu ya upungufu wa mvua katika msimu uliopita, hali ambayo ilichangia kushuka kwa mavuno ya zao la tumbaku miongoni mwa wakulima.

Hata hivyo, Majaliwa aliwataka watumishi wa wilaya hiyo, washirikiane na watendaji na madiwani ili kuongeza mapato ya wilaya hiyo badala ya kuwaachia watendaji wa kata peke yao.

Aidha, Majaliwa ameutaka uongozi wa mkoa wa Tabora uhakikishe wanapatikana watumishi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) katika wilaya hiyo ili waweze kusaidiana na watendaji wa halmashauri hiyo kukusanya mapato.

“Hapa Sikonge naambiwa hakuna ofisi za TRA. Lazima tupate maafisa wa TRA katika kila Halmashauri ili watoe elimu na washirikiane na madiwani, watendaji wa vijiji na watumishi wa Halmashauri juu ya ukusanyaji mapato,” alisema.

Picha: Rais Magufuli akutana na Bill Gates Ikulu Dar es salaam
Bill Gate atoa msaada wa mabilioni Tanzania