Kutokana na makanisa kuwa mengi, uendeshaji wa shughuli za ibada umekuwa kwa kasi kiasi cha kuwakwaza wakazi jirani na maeneo yanayozunguka makanisa hayo, kwani ibada zinazoendeshwa zimekuwa zikiambatana na muziki mkubwa, vilio na sauti mbalimbali ambapo kwa mujibu wa baadhi ya wakazi imeonekana kuwa kero.
Hivyo Mkuu wa Wilaya ya Musoma, Zelothe Stephen amefunguka na kusema uhuru wa kuabudu usifike mahala ukawa kero kwa wananchi wengine, hivyo ametoa tamko lililozingatia katiba na kusema kuwa, viongozi wa ibada inabidi wawe na ratiba maalumu kuhusiana na uendeshaji wa ibado hizo.
Amehoji na kusema kuwa ibada zinaendeshwa siku nzima wananchi wanapata wapi muda wa kufanya kazi kukidhi mahitaji ya familia zao, hivyo amewataka viongozi wa makanisa hayo wawe na muda maalumu wa kufanya ibada na si kuendesha ibada siku nzima huku wakiwa wamefungulia mziki kwa sauti kubwa kiasi cha kusumbua wakazi wa maeneo jirani.
Pia amesisitiza kwa viongozi wa makanisa hayo kupata kibali maalumu kutoka kwa serikali pindi wanapotaka kuendesha mikutano ya hadhara ili kutambua muda maalumu wa matukio hayo na kudhibiti usumbufu wa makelele utakaojitokeza kwa wananchi wengine.
Aidha wananchi walihojiwa kuhusu tamko hilo la mkuu wa wilaya, wapo waliunga mkono kwa madai kuwa kweli ibada hizo zinazoendeshwa kwa sauti ni chanzo cha makelele na kusabibisha wengi wao washindwe kupumzika vizuri usiku na mchana.
Pia baadhi ya wakazi wamepingana na tamko hilo na kumtaka mkuu wa wilaya kutafakari upya agizo hilo, kwani wanaamini kupitia uhuru huo wa kuabudu, wapo wanaoliombea taifa letu amani, na kuiombea serikali yetu utawala bora, kuingilia katiba na kwenda kinyume na katiba ya uhuru wa kuabudu ni uvunjifu wa sheria.