Katibu Mkuu wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania TUCTA, Yahya Msigwa amezungumza kwa niaba ya wafanyakazi wote hususani waliotumbuliwa katika sakata la vyeti feki na kuiomba serikali kuangalia upya hatua zilizochukuliwa juu ya watumishi hao na kuomba walipwe kifuta jasho.
Amesema kuwatoa katika ajira bila kuwapa chochote kunawafanya watunishi hao kuwa maskini ghafla, kwani maisha ya mtumishi ni mshahara wake.
Msigwa ameeleza kuwa endapo watalipwa kifuta jasho itawasaidia wale ambao bado wanamikopo kwenye mabanki na taasisi nyingine mbalimbali kuyapunguza.
”Kwa kuwatoa ghafla watumishi hao, hata benki zinaathirika kwani mikopo hairejeshwi hivyo suala hilo liangaliwe kwani zinaweza kufilisika kwa kutorejeshewa fedha zake, amesema Msigwa.
Aidha ameeleza kama TUCTA hawana ugomvi na serikali lakini wanaiomba iangalie jinsi ya kuwasaidia watumishi hao waliokumbwa na upepo wa vyeti feki, kwani kama TUCTA inatambua dhahiri kuwa kisheria ni makosa kwa mtumishi kuwa na cheti feki lakini inaomba swala hilo liangaliwe kwa jicho la tatu.
Yahya ametoa kauli hizo katika semina ya wataalamu wa kupitia sera za Ukimwi na Afya, Pia amelaumu mfumu uliokuwepo wakati huo pindi taasisi hizo za Serikali zinaajili watumishi.