Bosi wa RockStar4000, Ali Kiba amesema kuwa alikuwa hamuamini Ommy Dimpoz alipokuwa akimsikilizisha nyimbo zake walipokutana.

Ali ambaye ni Mkurugenzi wa lebo hiyo ambayo hivi karibuni ilimuongeza Ommy Dimpoz kama mwanafamilia mpya, ameiambia The Playlist ya 100.5 Times FM kuwa mara kadhaa walipokuwa wakikutana alikuwa akimsikilizisha nyimbo nzuri alizosema ameandika yeye, lakini kutokana na ukali wa nyimbo hizo alikuwa hamuamini.

“Ommy, mwanzoni nilikuwa kama simuamini-amini hivi. Akija na ngoma akiniimbia namuuliza ‘nani amekuandikia na nani amekupa hizi melodi?’ ananiaambia ‘ni mimi mwenyewe’. Nilikuwa siamini,” alisema Ali Kiba na kuongeza kuwa alipoisikia ‘Cheche’ alimuamini zaidi na kuamua kumvuta rasmi RockStar4000, kutokana na uimbaji wake.

“Kwenye ‘Cheche’ ameimba vizuri sana, na nilijaribu kumpa wazo kidogo na alilifanyia kazi. Lakini siwezi kusema ni sehemu gani na ni nini, ila niseme tu amenifurahisha na ameimba vizuri sana,” aliongeza.

‘Cheche’ ni wimbo wa kwanza wa Ommy akiwa kama mwanafamilia wa RockStar4000. Video ya wimbo huo bado haijatoka tofauti na ahadi aliyoitoa kwa mashabiki kuwa tayari ilikuwa imefanyika na inasubiri kutoka tu.

Hivi karibuni, Ali alisikika akisema kuwa video hiyo iko kwenye utaratibu wa kuboreshwa zaidi.

Msigwa alalamikia Serikali awaombea kifuta jasho wenye vyeti feki
Wazazi wajawa hofu, watoto watano watekwa