Serikali imeahidi kuendelea kufanyakazi bega kwa bega na sekta binafsi na kuthamini mchango wao ili kuhakikisha inafikiwa azma ya Tanzania ya Viwanda ambayo itainua uchumi wa nchi na wananchi.

Hayo yamesemwa hii leo jijini Dar es salaam na Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Philip Mpango alipokuwa akizindua kitabu cha Safari ya Tanzania kuelekea katika Uchumi wa Viwanda 2016- 2056, kilichoandikwa na watanzania wazalendo, Ali Mufuruki, Gilman Kasiga na Moremi Marwa.

‘’Kitabu hiki ni kama mkombozi kwa sisi watunga sera kwani kitatusaidia katika kuyafanyia kazi mapendekezo ambayo yametolewa ili kuhakikisha Tanzania ya viwanda inawezekana, nimewaelekeza pia Tume ya Mipango na Idara ya sera katika Wizara ya Fedha kuchukua mapendekezo ambayo wataona yataisaidia serikali katika kutekeleza azma yake ya kuendeleza viwanda’’amesema Dkt. Mpango

Aidha, kwa upande wake, Ali Mufuruki mmoja wa watunzi wa kitabu hicho amesema kuwa wameamua kuunganisha mawazo yao pamoja na kutumia utaalamu na uzoefu wao katika masuala mbalimbali ya maendeleo na uchumi ili kuisaidia serikali kuweza kuondokana na uchumi unaotegemea kilimo na hatimaye kuwa nchi ya viwanda.

Naye Gilman Kasiga ambaye pia ni Mkurugenzi wa Kampuni ya General Electric katika ukanda wa Afrika Mashariki, amesema ni vyema Tanzania ikawekeza katika masomo kwa kutambua vipaumbele kama inavyofanya nchi ya Ujerumani ambapo sio kila anayesoma ni lazima afikie ngazi ya shahada ndipo aonekane anaweza kuleta mchango katika maendeleo.

 

Manispaa ya Ubungo yazifungia shule 29
Kamati Ya Nidhamu Kuketi Kesho