Mbunge wa Sengerema, William Ngeleja ambaye amewahi kuwa Waziri wa Nishati na Madini wa awamu ya nne, leo Septemba 11 ameripoti katika ofisi ya Mkurugenzi wa upelelezi wa makosa ya jinai, DCI Robert Boaz.
Ngeleja ameitikia wito wa Mkuu wa Jeshi la Polisi IGP, Simon Sirro ambaye aliwataka watuhumia wote waliotajwa katika sakata la ripoti ya Tanzanite na Almasi wajisalimishe ofisini kwake kwa mahojiano zaidi.
Ngeleja ametumia muda wa saa moja kufanya mahojiano na DCI, ambapo kutokana na sababu za kiupelelezi hakuweza kuzungumza chochote kuhusu mahojiano yake na DCI, Robert Boaz.
Agizo hilo kwa mara ya kwanza lilitolewa na Rais John Pombe Magufuli pindi aliposomewa ripoti ya uchunguzi wa madini ya Tanzanite na Almasi.
Kupitia ripoti hiyo akaviagiza vyombo vya ulinzi na usalama kuwakamata mara moja wote waliotajwa katika ripoti hiyo.
Aidha Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za mitaa (TAMISEMI), George Simbachawene na Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Edwin Ngonyani, wameamua kujiuzulu kupisha uchunguzi wa vyombo vya dola.