Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Edward Lowassa amemtembelea mwanasheria mkuu wa chama hicho, Tundu Lissu anayepata matibabu katika hospitali ya Aga Khan jijini Nairobi nchini Kenya.

Lowassa ambaye ni waziri mkuu wa zamani, ameweka picha na ujumbe kwenye mtandao wa Twitter, picha inayomuonesha akiwa na Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe, mke wa Lissu anayefahamika kwa jina la Alicia na dereva wa Lissu, Simon Mohamed Bakari.

“Earlier today i paid a visit at Nairobi Hospital to see our MP, President of TLS and dear friend @tundulissutz. He is recovering well,” ametweet.

Kwa tafsiri isiyo rasmi, “mapema leo nilienda katika hospitali ya Nairobi kumuangalia mbunge wetu, Rais wa TLS na rafiki yetu mpendwa Tundu Lissu. Anaendelea vizuri.”

Katika tweet nyingine aliwaomba wananchi kuendelea kumuombea akieleza kuwa ni wakati wa masikitiko kwa Tanzania.

Lissu alipigwa risasi zaidi ya 30 na watu wasiojulikana akiwa ndani ya gari lake nyumbani kwake eneo la Area D mjini Dodoma, muda mfupi baada ya kurejea kutoka bungeni.


Kwa mujibu wa taarifa za madaktari, risasi tano zilimpata mbunge huyo wa Singida Mashariki na kwamba mbili zimempiga tumboni.

Juzi, Mbowe alisema kuwa Lissu anaendelea vizuri na ameweza kuzungumza maneno machache ambayo yalikuwa ujumbe wa kumtia moyo mwenyekiti huyo akimtaka kuendelea na mapambano na kwamba yeye amenusurika ili kusimulia mkasa.

Jeshi la Polisi linaendelea kuwasaka watu waliohusika na tukio hilo.

Serikali kudhibiti mfumuko wa bei ya mbolea nchini
Ngeleja ajisalimisha ofisi ya DCI kwa mahojiano