Wadau na Mashirika ya utetezi wa haki za binadamu nchini wamelaani tukio la kushambuliwa kwa risasi kwa Mbunge wa Singida Mashariki na Mwanasheria Mkuu wa Chadema, Tundu Lissu.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha kutetea haki za Binadamu (LHRC), Hellen Kijo Bisimba alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es salaam, ambapo amesema kuwa vitendo kama hivyo havivumiliki.
Amesema kuwa matukio mbalimbali ambayo yanaendelea kutokea nchini kwa sasa yameota sugu na kuonekana kama jambo la kawaida hivyo yanahitaji kukemewa hadharani bila woga.
“Sisi watetezi wa haki za binadamu tumekuwa tukifuatilia kwa ukaribu matukio mbalimbali ya kinyama, kikatili na yasiyokubalika yanayoendelea nchini kinyume cha haki za binadamu, tunalaani na tunakemea yasiendelee kutokea,”amesema Bisimba
Hata hivyo, ameongeza kuwa matukio hayo yanaota mizizi kwa kasi kubwa na kukosa ufumbuzi hivyo kusababisha hofu kubwa baina ya wapenda amani, watetezi wa haki za binadamu na wananchi kwa ujumla.