Serikali ya Uganda imezuia vyombo vya habari nchini humo kurusha moja kwa moja matangazo ya vikao vya bunge hilo kuanzia leo.
Marufuku hiyo imetangazwa na Mkurugenzi wa Tume ya Utangazaji nchini humo, Godfrey Mutabuzi.
Mutabuzi ameeleza kuwa sababu za kuweka marufuku hiyo ni za kiusalama zaidi.
Hatua hii imekuja ikiwa ni siku moja baada ya wabunge wa upinzani na wale wa chama tawala kupigana Bungeni. Vurugu hizo zilihusisha kurushiana viti na kuharibu baadhi ya vifaa vilivyokuwa ndani ya bunge hilo.
Ugomvi huo uliibuka wakati mswada wa kuondoa kifungu cha ukomo wa umri wa kuwania urais wa nchi hiyo ulipowasilishwa bungeni. Wabunge wa upinzani walipinga na kuanza kuimba wimbo wa Taifa bila ukomo. Vurugu hizo zilifanyika juzi na jana.
Spika wa Bunge, Rebecca Kagada alilazimika kuahirisha vikao vya bunge na kutoa adhabu ya kuwaondoa bungeni baadhi ya wabunge waliokutwa na hatia ya kuhusika moja kwa moja na vurugu hizo.