Ofisi za kampuni ya mfanyabiashara, Yusufu Manji zimefungwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kutokana na kudaiwa Shilingi bilioni 12.2.

Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipakodi, Richard Kayombo amesema wamekuwa na mawasiliano na kampuni ya ‘Farm Equipment’ inayomilikiwa na Manji tangu Agosti 15 mwaka huu lakini hakukuwa na mrejesho kuhusu deni hilo.

Amesema kutokana na hilo wamefunga ofisi zake kwa sababu kampuni hiyo inadaiwa kiasi cha Sh12.2 bilioni, lakini kampuni hiyo ina nafasi ya kuendelea kuwasiliana na TRA namna ya kulipa deni hilo.

TRA na kampuni ya udalali ya Yono waliambatana na polisi kwenda katika jengo hilo lililopo barabara ya Pugu, wilayani Temeke.

Wakiongea na mwananchi, baadhi ya mashuhuda wakiwamo walinzi kwa masharti ya kutotaja majina yao wameiambia Mwananchi kuwa ofisi zilizofungwa ni ya Manji na sehemu yake duka la kuuza pikipiki na matrekta.

Wamesema baada ya kufika watu waliingia moja kwa moja katika ofisi yake kisha kufanya majadiliano na wahusika yaliyodumu zaidi ya saa 2.

“Nadhani hawakufikiana mwafaka kwa sababu walivyotoka wakaamuru wafanyakazi wa ofisi hiyo kutoka nje kisha kuweka utepe wa rangi nyekundu na nyeupe,” amesema shuhuda huyo.

Mashuhuda hao wamesema hawajui tatizo ni nini lakini waliwasikia maofisa wa TRA na kampuni hiyo ya udalali wakizungumza kuhusu kodi.


Video: HATARI!! “Tulivunja shule baada ya kukosa hela, wazazi wangu walinifanyia kitu cha ajabu sana”

Magazeti ya Tanzania leo Oktoba 3, 2017
Diamond asherehekea siku ya kuzaliwa Amana, asimamisha shughuli