Beki wa Simba SC, Salum Mbonde amerejea uwanjani baada ya kupona majeruha ya goti aliyoyapata wakati wa mchezo wa ligi kuu ya soka Tanzania bara dhidi ya Mtibwa Sugar ya Morogoro.
Hatua hiyo imekuja ikiwa ni siku chache baada ya kuelezwa kuwa, Klabu ya Simba imeachana na beki kutoka nchini Zimbabwe Method Mwanjali, kupitia dirisha dogo la usajili ambalo lilifungwa rasmi Desemba 15.
Mbonde alisajiliwa na Simba SC mwezi Julai mwaka huu akitokea Mtibwa Sugar, na tayari ameonyesha uwezo mkubwa katika kikosi cha wekundu hao tangu alipoanza kucheza kwenye kikosi cha kwanza cha Joseph Marious Omog.
Hata hivyo Mbonde amesema wakati akiwa majeruhu alikua kifuatilia ligi kuu na kubaini ligi hiyo ina ushindani mkubwa, hivyo kurejea kwake tena uwanjani, kunamfanya aongeze bidii katika mazoezi ili kuweza kucheza soka katika kiwango cha juu zaidi na kuisaidia klabu yakeya Simba, ambayo itaendelea na ligi kuu Desemba 30 kwa kucheza na Ndanda FC mkoni Mtwara.
“Nashukuru nimepona na sasa nipo fiti, natarajia kurudi uwanjani wakati ligi itakapoendelea lakini nalazimika kufanya mazoezi ya nguvu ili kujiweka fiti kwa ajili ya kumudu ushindani uliopo,” amesema Mbonde.
Beki huyo amesema amejipanga kufanya mazoezi hayo kwa wiki nzima ili hadi ligi itakapoanza aweze kuwa fiti na kuendelea na kazi yake ya kulinda lango la Simba ambayo imepania kutwaa ubingwa wa Tanzania bara msimu huu.
Kurejea kwa Mbonde kunapunguza idadi ya majeruhi wa timu hiyo ukiachana na beki Shomari Kapombe na kipa Said Mohamed wanaoendelea na matibabu mpaka sasa.