Gwiji wa klabu ya Arsenal Robert Pires amempongeza meneja mpya wa klabu hiyo Unai Emery kwa kufanya maboresho katika kikosi chake, kuelekea msimu mpya wa ligi ya nchini England.
Pires ambaye alikuwa sehemu ya kikosi cha Ufaransa kilichotwaa ubingwa wa dunia mwaka 1998, ametoa pongezi kwa meneja huyo, kwa kuamini maboresho aliyoyafanya katika kikosi yanaonyesha dalili za kuleta ushindani dhidi ya klabu nyingine shiriki katika ligi.
Amesema kikosi cha Arsenal kilikua kinahitaji wachezaji wapya kwa muda mrefu, na kusajiliwa kwa wachezaji zaidi ya watatu, kutaleta ushindani baina ya wachezaji wanaocheza nafasi moja, jambo ambalo hapo awali halikuwepo.
Hata hivyo kauli hiyo ya Pires ambaye aliitumikia Arsenal kuanzia mwaka 2000 hadi 2006, inapingana na ile ya bosi wake wa zamani Arsene Wenger ambaye majuma mawili yaliyopita alikaririwa na vyombo vya habari akipinga sera ya usajili inayoendeshwa na meneja Unai Emery akisaidiana na mtendaji mkuu Ivan Gazidis.
“Unai Emery amefanya usajili mzuri mpaka sasa, ninaamini kutakua na mabadiliko makubwa katika kikosi cha Arsenal msimu ujao, jambo hili halikuzoeleka klabuni hapa kwa kipindi kirefu, na mashabiki walikata tamaa mapema kutokana na usajili hafifu uliokua ukifanywa,” alisema Pires alipohojiwa na Sky Sports News.
“Unai Emery ameshatwaa mataji akiwa Hispania, Ufaransa na anataka kulifanya jambo hilo hapa England.”
Kiungo kutoka nchini Uruguay Lucas Torreira na kinda la Ufaransa Matteo Guendouzi walikua wachezaji wa mwisho kusajiliwa klabuni hapo juma lililopita, huku kiungo aliedumu kwa kipindi kirefu Jack Wilshere akiondoka na kujiunga na majirani West Ham United.
Emery tayari ameshaonyesha makali yake katika mchezo wa kwanza wa kirafiki uliochezwa mwishoni mwa juma lililopita dhidi ya Boreham Wood, ambao walikubali kichapo cha mabao manane kwa sifuri.
Mchezo wa pili wa kirafiki kwa kikosi cha Arsenal unatarajiwa kuchezwa mwishoni mwa juma lijalo dhidi ya Atletico Madrid huko Singapore.
Emery mwenye umri wa miaka 46, ana jukumu zito la kuipatia mafanikio klabu ya Arsenal kwa kuhakikisha inamaliza katika nafasi za juu kwenye msimamo wa ligi msimu wa 2018/19, sambamba na kuifikisha mbali kwenye michuano ya Europa League.