Klabu ya Newcastle United imemsajili beki kutoka nchini Uswiz Fabian Schar kwa mkataba wa miaka mitatu, hatua ambayo inaendelea kudhihirisha ni vipi meneja wa klabu hiyo Rafael Benitez alivyojizatiti kwa msimu ujao wa ligi ya England.
Beki huyo mwenye umri wa miaka 26 amejiunga na Newcastle Utd akitokea Deportivo La Coruna ya nchini Hispania kwa ada ya Pauni milioni 3 ambazo ni sawa na dola za kimarekani milioni 3.96.
Msimu uliopita Schar aliitumikia Deportivo katika michezo 25 ya ligi ya Hispania, baada ya kusajiliwa na klabu hiyo akitokea Hoffenheim ya Ujerumani mwaka mmoja uliopita.
“Ninatarajia kuanza mazoezi na kikosi cha timu wakati wowote kuanzia sasa, nipo tayari kwa mapambano ya kuwania nafasi ya kucheza kwenye kikosi cha kwanza,” alisema beki huyo.
Schar alicheza michezo mitatu ya fainali za kombe la dunia akiwa na timu ya taifa lake la Uswiz, na alikua miongoni mwa wachezaji walioonyesha uwezo mkubwa ambao ulisaidia kuifikisha timu hiyo hatua ya 16 bora kabla ya kufungwa na Sweden.