Wataalamu wa afya ya uzazi na magonjwa ya zinaa wamebaini kuwa kuna baadhi ya watu wamekuwa wakifanya yasiyotarajiwa, kwa kufua kondom baada ya kuzitumia kwa tendo la ndoa, kuzianika na kisha kuzitumia tena!
Tabia hii ambayo awali iliaminika kuwa huenda ni utani tu, imebainishwa kufanyika baada ya taasisi ya kuzuia magonjwa ya zinaa ya Centers for Disease Control (CDC) ya Atlanta Marekani kuchukua hatua ya kutoa elimu husika.
Bila kutaja jamii waliyoibaini kuwa hufua kondomu na kuzianika kama nguo, CDC wamewataka watu wote kutofanya hivyo kwani kondomu moja hutumika kwa tendo moja tu.
“Tunasema kwa sababu watu wanafanya hivi; usifue au kutumia tena #kondom ambazo umezitumia! Tumia kondom mpya mara moja kwa kila tendo moja,” CDC wameandika kupitia Twitter na kuambatisha ‘link’ yenye maelezo ya kina.
We say it because people do it: Don’t wash or reuse #condoms! Use a fresh one for each #sex act. https://t.co/o3SPayRf9m pic.twitter.com/AwkPqE9YMl
— CDC STD (@CDCSTD) July 23, 2018
Mtaalam wa tiba wa CDC Idara ya Kuzuia Maambukizi ya Magonjwa ya Zinaa, Elizabeth Torrone amefanya mahojiano na CNN na kueleza kuwa wamebaini kuwepo kwa suala hilo na kuamua kulitolea ufafanuzi.
“Kondom huzuia kusambaa kwa magonjwa mengi ya zinaa na hupunguza hatari ya magonjwa yote ya zinaa, lakini kondomu itafanya kazi kama tu itatumika kwa usahihi,” alisema.
“Kutotumia kondom kwa usahihi kama vile kuziosha na kutumia tena kunaweza kusababisha kupasuka, kuvulika au kuchanika,” aliongeza.
Usichukulie poa, elimu ya matumizi ya kondom bado inahitajika sio tu kutumia bali pia namna sahihi ya kutumia. Inaelezwa kuwa ni idadi ndogo sana ya watu husoma maelekezo ya jinsi ya kutumia kondom, iwe ni mijini au vijijini, ikiwa ni pamoja na kuangalia kama muda wake umekwisha (expiry date). Tukumbushane!