Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam inawashikilia watu wawili kwa tuhuma za kuteka watu na kudai fedha kiasi cha Shil. 60 milioni kwa ndugu wa waliotekwa.

Watuhumiwa hao ambao ni pamoja na Hussein Shilingi mkazi wa Kimara na Martine Pumba mkazi wa Tabata wote walikamatwa Julai 26 mwaka huu maeneo ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) wakitumia gari aina ya Toyota Land Cruiser yenye namba ya Umoja wa Mataifa (UN) huku wakiwa na watu watano waliowateka.

Hayo yamesemwa na Kamanda wa Polisi kanda hiyo Lazaro Mambosasa alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari, ambapo amesema kuwa baada ya kufanya upekuzi ndani ya gari hilo walifanikiwa kukamata vifaa mbalimbali vilivyokuwa vikitumiwa na wahalifu hao ikiwamo namba za magari za mashirika ya serikali, Umoja wa Mataifa na namba za binafsi.

“Hawa watekaji walikuwa wanatumia gari moja lakini walikuwa wanabadilisha namba tofauti za magari kama za serikali, ubalozi na za umoja wa kimataifa ili mtu usiweze kuwagundua na pia walikuwa wanatembea na matunguli wakiamini hawakamatwi lakini wajue Serikali hailogwi hata siku moja na tunaendelea kumtafuta mganga wao wa kienyeji,”amesema Mambosasa.

Hata hivyo,  Mambosasa amesema kuwa vitu vingine walivyokamata ni kitambulisho cha kugushi chenye nembo ya polisi chenye jina la Martin Pumba simu za mkononi, silaha ikiwamo panga, nondo sime na maganda matatu ya risasi yanayodhaniwa kuwa ni ya bunduki aina ya SMG.

Ni moto: McGregor arejea ulingoni UFC, mpinzani wake ana kisasi
Wanaofua kondom na kutumia tena 'wafundwa'