Macho yameelekezwa kwenye kesi ya kupinga matokeo ya uchaguzi mkuu wa Zimbabwe ilivyofunguliwa na aliyekuwa mgombea wa MDC, Nelson Chamisa.
Kesi hiyo inayoendelea leo kwenye Mahakama Kuu nchini humo mbele ya jopo la Majaji watatu, itahitimishwa kwa kuamua kuhalalisha au kubatilisha matokeo ya uchaguzi yaliyompa ushindi wa asilimia 50.8, Rais wa Zimbabwe, Emmerson Mnangagwa.
Wakili kiongozi wa Chamisa, Thabini Mpofu amesoma kiapo cha aliyekuwa wakala wa Chamisa akieleza kuwa alifanyiwa vitendo viovu ikiwa ni pamoja na mumewe kulawitiwa siku ambayo kura zilikuwa zinahesabiwa.
Mpofu akisoma kiapo hicho, alisema kuwa wakala huyo mwanamke alisema alifukuzwa kwenye kituo cha kupigia kura na aliruhusiwa kurejea baadaye baada ya zoezi la kuhesabu kura na kwamba alilazimishwa kusaini fomu namba V11 ya matokeo lakini alikataa.
Aliongeza kuwa wakala huyo alielekea nyumbani kwake lakini kabla hajaingia ndani alibaini kuwa anafuatiliwa na watu waliokuwa wamejifunika sura zao. Alisema watu hao walimvamia na kumshambulia na kisha kumlawiti mume wake.
Katika ushahidi mwingine, Mpofu alionesha kablasha ambalo ndani yake lilikuwa na fomu namba V11 ambazo zilikuwa zimesainiwa na kugongwa mihuri sahihi lakini hazikuwa zimejazwa taarifa za idadi ya kura.
Mpofu amedai kuwa fomu hizo zisizo na taarifa ziliwekwa hivyo ili kusaidia kujaza taarifa za uongo na za uchakachuaji hapo baadaye.
Aidha, muwakilishi wa Tume ya Uchaguzi ya ZEC alikiri kuwepo kwa kasoro za kimahesabu kwenye matokeo yao.
Wakili mwingine wa Chamisa, Sylvester Hashiti alidai kuwa kama mahesabu yalikuwa na makosa ni dhahiri kuwa matokeo yaliyotangazwa yalikuwa na makosa pia.
Mawakili wa Chamisa wanadai kuwa matokeo ya uchaguzi hayakuwa halali kwani hayakuthibitishwa, hivyo wanaiomba mahakama kubatilisha matokeo yaliyotangazwa na tume.
Kesi inaendelea, upande wa Tume ya Uchaguzi bado haujaanza kuwasilisha utetezi wake pamoja na chama cha Zanu PF.